Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi awaasa watendaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo ya Tume

Imewekwa: 16 Jul, 2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi awaasa watendaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo ya Tume

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewaasa watendaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume.

Hayo yamesemwa mkoani Morogoro na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele wakati akifungua mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu kwa tarehe itakayotangazwa na Tume.

Mhe. Jaji Mwambegele amewataka watendaji hao wajitahidi na wajiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kwa khakikisha wanazingatia ipasavyo Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo ya Tume.

 "Jitahidini na mjiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi. Hakikisheni mnazingatia ipasavyo Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume," amesema Mhe. Jaji Mwambegele.

Amewasisitiza watendaji hao kuvishirikisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika hatua zote kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, sheria, kanuni na maelekezo ya Tume na kwamba ni muhimu kuwashirikisha wadau hao kwenye maeneo wanayopaswa kushirikishwa kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo ya Tume.

Mhe. Jaji Mwambegele amewakumbusha kutambua wajibu wao ikiwemo kuvitambua vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika na kuhakikisha kunakuwa na mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.

"Ajira za watendaji wa vituo zizingatie kuajiri watendaji wenye weledi, wanaojitambua, wazalendo, waadilifu na wachapakazi na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi," amesema Jaji Mwambegele.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk amefungua mafunzo ya watendaji hao Mjini Unguja, Zanzibar ambapo amewasisitiza watendaji hao kuhakikisha vifaa vya uchaguzi wanavyopokea kutoka Tume, wanavihakiki, kuvikagua na kuhakikisha vinasambazwa kwenye vituo vyote.

"Wakati wa kuapisha mawakala, toeni taarifa mapema kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo ya Tume na kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura ili kuviwezesha kupanga mawakala," amesema Jaji Mbarouk.

Amewataka kuhakikisha kuwa siku ya uchaguzi wanaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 kamili asubuhi na kufanya mawasiliano na Tume pale ambapo ushauri utahitajika kuhusiana na masuala ya uchaguzi.

Naye Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari, akifungua mafunzo kwa watendaji wa Uchaguzi Mkuu ngazi ya Jimbo kwa Mkoa wa Geita na Kagera, amewasisitiza watendaji hao kuvishirikisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika hatua zote muhimu wanazopaswa kushirikishwa kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria, Kanuni na maelekezo mbalimbali ya Tume.

Wakati huo huo Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Balozi Omar Ramadhan Mapuri, naye, amefungua mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Aidha, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe.Magdalena Rwebangira akifungua mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi wa mikoa ya Tabora na Kigoma, amewstaka watendaji wa Uchaguzi kusoma kwa makini Katiba, Sheria, Kanuni, Miongozo na maelekezo ya Tume na kuyatumia vyema mafunzo hayo kupata ufafanuzi wa maeneo yenye changamoto.

"Someni kwa umakini katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na Maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume na ulizieni ili mpate kufafanuliwa kwenye maeneo ambayo kwa namna moja au nyingine kutakuwa na changamoto" alisema Mhe.Rwebangira.

Mafunzo haya ya siku tatu yanatarajia kukamilika tarehe 17 Julai, 2025 huku yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo watendaji wa Uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa

Ambao ni waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo.

Tume imeyagawa mafunzo hayo kwenye awamu mbili ambapo awamu hii ya kwanza inahusisha watendaji kutoka mikoa ya Morogoro, Singida, Dodoma, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Mjini Magharibi, Geita, Kagera, Mtwara, Lindi, Tabora, Kigoma, Tanga, Kilimanjaro, Ruvuma, Iringa na Njombe.