Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Menejimenti ya INEC yajengewa uwezo wa utekelezaji wa mikataba kupitia NeST.

Imewekwa: 28 Jun, 2026
Menejimenti ya INEC yajengewa uwezo wa utekelezaji wa mikataba kupitia NeST.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA)Bw.Dennis Kwame Simba leo tarehe 27 Juni, 2026 amefungua mafunzo ya siku tano kwa Menejimenti ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu sheria ya ununuzi wa Umma na matumizi ya mfumo wa NeST yanayofanyiKa katika Ukumbi wa Bohari Jijini Dar es Salaam.

 

Bw.Simba katika hotuba yake ya ufunguzi amesema kuwa mfumo wa kidijitali wa ununuzi wa umma (NeST) umekuwa mkombozi mkubwa kwa kuongeza uwazi, uwajibikaji, na kudhibiti udanganyifu ikiwemo matumizi ya nyaraka za kughushi kwenye michakato ya zabuni nchini.

 

​Ameongeza kuwa mfumo huo umekuja kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya ununuzi kwa kuhakikisha Taasisi nunuzi na wazabuni wote wanawajibika kikamilifu kulingana na sheria na miongozo iliyopo.

 

​"Mfumo wa NeST umesaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa taarifa sahihi na za kuaminika kwa wakati, jambo ambalo limeondoa kabisa mianya ya matumizi ya nyaraka za kughushi zilizokuwa zikijitokeza huko nyuma," amesisitiza Bw.Simba.

 

 

​Mbali na kudhibiti udanganyifu na kuimarisha uwazi, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw.Simba amebainisha faida nyingine za kiikolojia na kiuchumi za mfumo huo, akisema umepunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya karatasi katika ofisi za serikali, hatua inayoongeza utunzaji wa kumbukumbu.

 

​Bw.Simba amewahimiza washiriki  kufuatilia mafunzo hayo kwa umakini mkubwa ili kupata uelewa wa kina utakaosaidia kurahisisha utekelezaji wa mikataba ya zabuni na kuleta tija katika taasisi hiyo muhimu.

 

Awali wakati akimkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima R.K alisema ​Mafunzo haya yanafanyika kwa lengo la kuwajengea uwezo Menejimenti na watumishi wa INEC kuendesha michakato ya ununuzi kwa ufanisi wa hali ya juu na kwa kuzingatia viwango vya kisasa vya kidijitali.