Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mjumbe wa INEC, Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari ametembelea na kukagua maandalizi ya Uchaguzi mdogo wa Udiwani Kata ya Shiwinga, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe

Imewekwa: 21 Feb, 2026
Mjumbe wa INEC, Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari ametembelea na kukagua maandalizi ya Uchaguzi mdogo wa Udiwani Kata ya Shiwinga, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari leo tarehe 21 Februari, 2026 ametembelea na kukagua maandalizi ya Uchaguzi mdogo wa Udiwani Kata ya Shiwinga, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe.

Akiwa kwenye ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbozi, Mhe. Asina  amezungumza na watendaji wa uchaguzi ngazi ya Mkoa na Jimbo la Mbozi na kisha baadaye akakagua maandalizi ya uchaguzi huo katika Kata ya Shiwinga.

Amewakumbusha watendaji hao kuzingatia Sheria, Kanuni na maelekezo ya Tume katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo kufanikisha uratibu wa mawakala wa vyama vya siasa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwenye vituo vya kupigia kura. 

“Kuhusu suala la mawakala wa vyama vya siasa, niwakumbushe kufuata Sheria, Kanuni na maelekezo ya Tume, tuepuka kudai barua ya utambulisho wakati Tume imeshatoa maelekezo ya namna nzuri ya kuwapata na kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao”, amesema Mhe. Asina.

Amesisitiza suala la vifaa vya uchaguzi lifanyike kwa makini kwa kuzingatia mahitaji ya kila kituo cha kupigia kura na kwamba watendaji hao wawasisitize wasimamizi wa vituo vya kupigia kura wakague na kuvihakiki vifaa vyote ili kuepusha usumbufu wakati wa uchaguzi.

Amesema Tume imetoa kibali kwa waangalizi wa uchaguzi kwa ajili ya kuangalia uchaguzi huo, hivyo, wapiga kura wanapaswa kupewa taarifa juu ya uwepo wa wadau hao. 

Aidha amewakumbusha watendaji hao kushirikiana na taasisi na asasi za kiraia zilizopewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na kutumia njia mbalimbali kutoa elimu hiyo ili kufanikisha uchaguzi huo.

Amewataka watendaji hao kuhakikisha wanabandika mabango na matangazo ya uchaguzi katika maeneo husika na kutoa matangazo kwa wapiga kura kwani hiyo ni njia muhimu ya kuwapa taarifa wananchi ili waweze kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huo.

Mhe. Asina amewapongeza watendaji hao wa uchaguzi katika Kata ya Shiwinga kwa namna wanavyovishirikisha vyama vya siasa katika hatua zote za uchaguzi, jambo ambalo limefanya maandalizi ya uchaguzi huo kwenda vizuri hadi kufikia sasa.

Kwa upande wake Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Kata ya Shiwinga, Bw. Selestin Lwambano amesema maandalizi ya uchaguzi huo yanakwenda vizuri hadi sasa kwani vifaa vya uchaguzi vimeshafika ngazi ya Kata na kampeni za uchaguzi zinaendelea vizuri.

Kuhusu mawakala wa vyama vya siasa, Bw. Lwambano amesema vyama vya siasa vimewasilisha mawakala wao na wameshaapishwa kutekeleza majukumu yao.