Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Wagombea 108 kutoka vyama vya siasa 17 kuwania ubunge na udiwani katika Uchaguzi Mdogo wa Ubuge katika Jimbo la Ismani na kata 12 za Tanzania Bara

Imewekwa: 31 May, 2026
Wagombea 108 kutoka vyama vya siasa 17 kuwania ubunge na udiwani katika Uchaguzi Mdogo wa Ubuge katika Jimbo la Ismani na kata 12 za Tanzania Bara

Jumla ya wagombea 108 kutoka katika vyama vya siasa 17 wanatarajiwa kuwania nafasi wazi ya ubunge na udiwani katika Uchaguzi Mdogo wa Ubuge katika Jimbo la Ismani lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Iiringa Mkoa wa Iringa na kata 12 za Tanzania Bara utakaofanyika kesho siku ya Jumatatu tarehe 1 Juni, 2026.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs C. M. Mwambegele leo siku ya Jumapili tarehe 31 Mei, 2026 Mkoani Iringa, wakati akitoa Risala kuhusu zoezi la kupiga kura kwenye Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Ismani na Madiwani Katika Kata 12 Za Tanzania Bara.

Amesema katika uchaguzi huo, Jimbo la Ismani lina wagombea 17 wa nafasi ya Ubunge ambapo kati ya wagombea hao wagombea nane (08) sawa na asilimia 47.06 ni wanaume na wagombea tisa (09) sawa na asilimia 52.94 ni wanawake. Kata 12 zinazofanya uchaguzi mdogo wa udiwani zina jumla ya wagombea 91 ambapo kati ya hao wagombea 61 sawa na asilimia 67.03 ni wanaume na wagombea 30 sawa na asilimia 32.97 ni wanawake.

Kutokana na takwimu hizo,  Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs C. M. Mwambegele kwa namna ya pekee, amevipongeza vyama vya siasa na wagombea waliojitokeza kushiriki katika uchaguzi huo.

Mhe. Jaji Mwambegele aidha, amesema jumla ya wapiga kura 222,218 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura watashiriki kwenye uchaguzi huo ambapo wapiga kura 89,753 wapo kwenye Jimbo la Ismani na wapiga kura 132,465 wapo kwenye kata 12 zitakazofanya uchaguzi mdogo.  

Kuhusu vituo vya kupigia kura, Mhe. Jaji Mwambegele amesema jumla ya vituo 628 vya kupigia kura vitatumika ambapo vituo 277 vipo kwenye Jimbo la Ismani na vituo 351 vipo kwenye kata 12 zitakazofanya uchaguzi mdogo.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs C. M. Mwambegele amevikumbusha vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo mdogo utakaofanyika kesho tarehe 01 Juni, 2026 kuzingatia wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupiga, kuhesabu na kujumlishia kura.

Amesema wasimamizi wa uchaguzi katika jimbo na kata husika, wamekamilisha taratibu zinazoweka mazingira yanayowawezesha mawakala wa vyama vya siasa kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi.

“Mawakala hao, wanawajibika kuwakilisha na kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao. Hivyo, wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu za Uchaguzi na maelekezo ya Tume katika utekelezaji wa majukumu yao vituoni.”, ameongeza Mhe. Jaji Mwambegele.

Amevikumbusha vyama vya siasa, wagombea, mawakala, wapiga kura na wananchi wote kwa ujumla kuzingatia kuwa mpiga kura, anatakiwa kwenda katika kituo alichojiandikisha na kadi yake ya mpiga kura siku ya uchaguzi.

Amefafanua kuwa wapiga kura watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Na mpiga kura awapo kituoni anatakiwa kutoa kipaumbele kwa wapiga kura wenye mahitaji maalumu kama vile wazee, wagonjwa, watu wenye ulemavu, wajawazito na akina mama wenye watoto wachanga watakaokuwa nao kituoni.

“Watu wenye mahitaji maalumu wanaruhusiwa kwenda kituoni na wasaidizi wao. Vituo vitafunguliwa saa 01:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Ifikapo muda wa kufunga kituo saa 10:00 kamili jioni, kama wapiga kura bado wapo kwenye mistari, mlinzi wa kituo atasimama nyuma ya mtu wa mwisho na zoezi la upigaji kura litaendelea hadi wapiga kura waliopo kwenye mstari watakapomalizika. Mpiga kura atakayefika zaidi ya muda wa kufunga kituo hataruhusiwa kupiga kura”, amesistiza Mhe. Jaji Mwambegele.

Mhe. Jaji Mwambegele amewasisitiza wapiga kura kuwa, baada ya kumaliza kupiga kura, mpiga kura anatakiwa kuondoka eneo la kituo cha kupigia kura na kwamba mpiga kura awapo kituoni, anatakiwa kufuata maelekezo yote atakayopewa na karani mwongozaji wapiga kura. 

Ameongeza kuwa, kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 4, 14(2), 19(3), 84(3)(a) na (b) na 164 vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343, vikisomwa pamoja na kifungu cha 26 cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 292, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ilitoa maelekezo ya kisera katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa wapiga kura.

Amesema maelekezo hayo  ni kwa mpiga kura asiye na picha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lakini ana kadi ya Mpiga Kura yenye taarifa binafsi zilizomo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ARUHUSIWE KUPIGA KURA.

Ameongeza kuwa kwa mpiga kura ambaye ana kadi yenye namba ya mpiga kura inayotofautiana na namba ya mpiga kura iliyomo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lakini taarifa nyingine zote ikiwemo picha na majina yaliyopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni sawa kama ilivyo katika kadi ya mpiga kura aliyonayo; ARUHUSIWE KUPIGA KURA.

Aidha Mhe. Jaji Mwambegele amesisitiza kuwa kwa mpiga kura ambaye ameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na taarifa zake zipo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililopo katika kituo husika, lakini amepoteza kadi yake au kadi yake imeharibika, ARUHUSIWE KUPIGA KURA kwa kutumia mojawapo ya vitambulisho vituatavyo.

Amevitaja vitambulisho hivyo kuwa ni Kitambulisho cha Taifa (NIDA); Leseni ya udereva; au Pasi ya kusafiria (Passport) Lakini kwa sharti kwamba, majina yake yaliyopo katika kitambulisho atakachowasilisha mpiga kura, ni lazima yafanane na majina yote kama yalivyo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Amesema kwa mpiga kura ambaye ana kadi ya kupigia kura lakini taarifa zake hazipo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ASIRUHUSIWE KUPIGA KURA.

Hivyo, Mhe. Jaji Mwambegele amewakumbusha wote kuzingatia maelekezo haya ya kisera. imetoa rai kwa wapiga kura kwenye maeneo yenye uchaguzi, kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura hapo kesho, ili kuwachagua viongozi wanaowataka.