Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Asina Omari awaaasa watendaji wa uboreshaji wa Daftari kuvitunza vizuri vifaa vya uboreshaji ili kufanikisha zoezi hilo

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari amefunga mafunzo ya uboreshaji wa Daftari kwa Waratibu, Waandishi Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya Bayometriki wa Vyuo vya Mafunzo Kisiwani Unguja, Zanzibar na kuwaasa watendaji hao kuhakikisha kuwa wanavitunza vizuri vifaa vya uboreshaji wa Daftari.
“Mnasisitizwa kuzingatia kwa umakini utunzaji wa vifaa vya uandikishaji kwa kuwa vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana. Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa ya vifaa hivyo muhimu kwa Taifa,” amesema Jaji Asina.
Amewakumbusha watendaji hao juu umuhimu wa kuzingatia muda sahihi wa kufungua na kufunga vituo vya kuandikisha wapiga kura na kuongeza kuwa watendaji hao wanapaswa kuwa na matumizi ya lugha nzuri kwa wale watakaowahudumia vituoni.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume, zoezi hilo la uboreshaji wa Daftari kwenye Magereza na Vyuo vya Mafunzo linafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 28 Juni hadi tarehe 04 Julai, 2025 ambapo watakaohusika ni mahabusu, wafungwa na wanafunzi waliohukumiwa kifungo chini ya miezi sita.
Naye Mjumbe wa INEC, Mhe. Balozi Omar Ramadhan Mapuri mkoani Dodoma akifunga mafunzo kama hayo Jijini Dodoma kwa Tanzania Bara amewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari kuzingatia mafunzo waliyopatiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ili waweze kutekeleza zoezi hilo kwa ufanisi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika ikiwa ni maandalizi ya kuandikisha na kuboresha taarifa za mahabusu, wafungwa na wanafunzi waliohukumiwa kifungo chini ya miezi sita.
“Ikumbukwe kwamba, mafunzo na maelekezo mliyopewa ni zana muhimu za kuwawezesha kutekeleza kwa ufanisi majukumu yenu. Hivyo, mnatakiwa kuyafahamu vizuri na kuyafuata ili kutekeleza zoezi hili kwa ufanisi. Someni kwa makini vitabu vya maelekezo mlivyopatiwa ili kazi yenu ifanyike kwa usahihi,” amesema Mhe. Mapuri.
Amewasisitiza watendaji hao juu ya umuhimu wa kuwasiliana na waratibu kwa ajili ya ufafanuzi wa masuala yote yanayohusiana na utekelezaji wa majukumu yao.