Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, awataka wananchi wa Mkoa wa Tabora kujitokeza kuhakiki na kuboresha taarifa zao katika uboreshaji wa Daftari

Imewekwa: 05 May, 2025
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, awataka wananchi wa Mkoa wa Tabora kujitokeza kuhakiki na kuboresha taarifa zao katika uboreshaji wa Daftari

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndg. Ramadhani Kailima amewataka wananchi wa Mkoa wa Tabora kujitokeza kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuhakiki taarifa zao katika uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura kwenye vituo walivyojiandikishia na kutoa taarifa za wale waliopoteza sifa za kuwemo kwenye daftari hilo.

Ndg. Kailima ameyasema hayo tarehe  4 Mei, 2025 wakati alipokuwa anatembelea na kukagua vituo vya kuandikisha wapiga kura katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ambapo amesema wananchi wameonesha mwitikio mkubwa kwa kujitokeza kuhakiki taarifa zao.

Amesema Tume imeweka wazi daftari la awali la wapiga kura katika vituo vyote vilivyotumika kuandikisha wapiga kura katika awamu ya pili hivyo wananchi wajitokeze kuhakiki taarifa zao na kutoa taarifa za wale ambao hawastahili kuwemo katika daftari hilo.

 

“Wananchi endapo wataona katika Daftari ambalo tumeliweka katika kila kituo kuna mwananchi ambaye amepoteza sifa kama vile kufariki basi wawe huru kwa kutumia fomu namba 5B kumuondoa huyo ambaye amepoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” amesema Kailima.

Ameongeza kuwa, Mkoa wa Tabora una vituo vya kujiandikisha wapiga kura 376 mkoa mzima na amewasisitiza wananchi waendelee kujitokeza katika kuboresha taarifa zao wale ambao hawakuboresha taarifa zao katika awamu ya kwanza ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Amefafanua kuwa Tume inatoa nafasi kwa watu wote wenye ulemavu wa macho na viziwi na wasiojua kusoma wanatakiwa kuja na watu wao wenye uwezo wa kuwasaidia ili waweze kujiandikasha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Kwa upande wake, Mratibu wa Uandikishaji Mkoa wa Tabora, Elihuruma Nyella amesema uboreshaji wa Daftari na uandikisha wa wapiga kura katika Mkoa wa Tabora unaendelea vizuri na watu wanaendelea kujitokeza.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili unafanyika sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura kuanzia Mei 01, 2025 na kukamilika tarehe 07, 2025 katika mikoa 15 ya mzunguko wa kwanza.