Mwenyekiti wa INEC Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele awataka Makarani waongozaji Wapiga kura kufanya kazi yao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za Uchaguzi
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amewataka watendaji wa vituo vya kupigia kura ambao ni Makarani waongozaji Wapiga kura kufanya kazi yao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu wakati wa uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Ismani, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mkoani Iringa na Kata 12 za Tanzania Bara.
Jaji Mwambegele ameyasema hayo wakati alipotembelea mafunzo ya siku moja kwa Makarani hao waogozaji katika Jimbo la Isimani yaliyofanyika katika Shule Sekondari Ufundi Ifunda mkoani Iringa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi huo utakaofanyika Jumatatu ya Juni 1, 2026.
Amewataka watakapokwenda kutekeleza majukumu yao wakazingatie mafunzo ambayo wamepewa na wakati wa kutekeleza majukumu hayo wafuate sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.
Jaji Mwambegele pia amewasisistiza watendaji hao kuishi kwenye viapo vyao wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya Uchaguzi ili kujiepusha na upendeleo wa aina yoyote.
“Nawasisitiza mtakapokwenda kutekeleza majukumu yenu mkakiishi kiapo chenu kwani kiapo hicho kinawaelekeza kuwa waaminifu kwa taifa lenu na kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi katika kutekeleza majukumu yaliyo mbele yenu”, amesema Jaji Mwambegele.
Naye mwenyekiti wa Mafunzo hayo ya Makarani Waongozaji Wapiga Kura, Baraka Matonya amemuhakikishia Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwamba watafuata sheria, kanuni, miongozo na maelekezo ya Tume wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao ya Uchaguzi .
Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Isimani, Caroline Otieno amesema maandalizi ya Uchaguzi Mdogo wa Jimbo hilo, yamekamilika kwa asilimia 100 ambapo vifaa vyote vimepokelewa.
Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Ismani utafanyika pamoja na Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata 12 za Tanzania Bara ambazo ni Mzimuni iliyopo Manispaa ya Kinondoni; Zongomera, Manispaa ya Kahama; Itilo, Halmashauri ya Mji wa Nzega; Ketare, Halmashauri ya Mji wa Tarime na Nyumbigwa, Halmashauri ya Mji wa Kasulu.
Nyingine ni kata ya Kala iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi; Ziba, Halmashauri ya Wilaya Igunga; Kamsisi, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele; Nyamugali, Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe; Namasakata Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru; Bwongera, Halmashauri ya Wilaya ya Chato na Kibiti Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.
“KURA YAKO HAKI YAKO, JITOKEZE KUPIGA KURA”

