Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi awataka wananchi wa mikoa 15 kutumia siku zilizobaki kujiandikisha, kuboresha na kuhakiki taarifa zao

Imewekwa: 05 May, 2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi awataka wananchi wa mikoa 15 kutumia siku zilizobaki kujiandikisha, kuboresha na kuhakiki taarifa zao

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amewataka wananchi wa mikoa 15 inayoshiriki Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili mzunguko wa kwanza na Uwekaji Wazi wa daftari la Awali la Wapiga Kura kuhakikisha kuwa wanajitokeza kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao kwa siku mbili zilizobaki ili wasikose haki yao ya msingi ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka huu.

Mhe. Jaji Mwambegele ameyasema hayo leo wakati akitembelea vituo mbalimbali vya kuandikisha wapiga kura katika halsmahauri mbalimbali za Mkoa wa Katavi.

“Nawasihi wananchi wa mikoa 15 ambayo awamu ya pili ya Uboreshaji Daftari inafanyika wandelee kujitokeza kuja kuboresha, waendelee kujiandikisha lakini pia kuwaondoa wale ambao hawastahili kuwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, tumebakiwa na siku chache zinazotakiwa kuendelea na zoezi,” amesema Jaji Mwambegele.

Ameongeza kuwa uboreshaji wa Daftari na Uwekaji Wazi wa Daftari la Awali unatoa fursa kwa wananchi kukagua, kufanya marekebisho ya taarifa za wapiga kura na uwekaji wa pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa na kwamba daftari la awali limebandikwa katika vituo vyote vilivyotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza.

Akizungumzia kuhusu mwenendo wa zoezi hilo kwa ujumla Mhe. Jaji Mwambegele amesema zoezi linakwenda vizuri na mwitikio wa wananchi ni mzuri kwani maeneo aliyotembelea katika mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma wananchi wamejitokeza vituoni kujiandikisha, kuboresha taarifa zao pamoja na kutoa taarifa za watu waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari.

“Kwa ujumla wake zoezi linakwenda vizuri na wananchi wengi wamejitokeza kwa ajili ya kuboresha taarifa zao, wamejitokeza pia, wale ambao hawastahili kuwepo katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura wamefutwa, katika kila kituo nil;ichokwenda wameniambia kuhusu wale walio waandikisha, waboresha na wale waliowafuta,” alisema.

Uboreshaji wa Daftari unafanyika kwa mizunguko mitatu ambapo mzunguko wa kwanza unajumuisha mikoa 15, mzunguko wa pili utajumuisha mikoa 16 na mzunguko wa tatu utajumuisha vituo vya magereza na vyuo vya mafunzo.

Mikoa inayohusika kwenye mzunguko wa kwanza wa uboreshaji ni Iringa, Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe ambapo zoezi hilo lilianza tarehe 1 Mei na linatarajia kukamilika tarehe 7 Mei, 2025. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Maafisa Waandikishaji kutoka Majimbo ya Nyasa, Ndg. Khalid Khalifa na wa Jimbo la Mbinga Mjini Ndg. Amina Hamisi Seif wamesema zoezi la uboreshaji wa Daftari katika maeneo yao linakwenda vizuri na kuwahimiza wananchi kuendelea kujitokeza.

“Kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa tumekwisha andikisha wapiga kura wapya 436 na kuboresha taarifa za wapiga kura 415 wakati wapiga kura 68 wamepoteza sifa na kufutwa katika Daftari, bado tuzazo siku hivyo nitumia fursa hii kuwaomba wananchi waendelee kujitokeza,” amesema Khalifa. 

Katika awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari, inatarajiwa wapiga kura wapya 1,396,609 wataandikishwa, wapiga kura 1,092,383 wataboresha taarifa zao na wapiga kura 148,624 watafutwa kwenye Daftari kwa kupoteza sifa za kuendelea kuwemo kwenye Daftari,” amesema Jaji Mwambegele.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetekeleza Uboresahji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Kwanza kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 hadi tarehe 25 Machi, 2025.