Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema uboreshaji wa Daftari kwenye magereza na vyuo vya mafunzo unaendelea vizuri

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili katika Mzunguko wa Tatu kwenye magereza ya Tanzania Bara na vyuo vya mafunzo kwa Tanzania Zanzibar, linaendelea vyema.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea magereza katika mikoa ya Kagera, Geita na Shinyanga, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema magereza yote aliyotembelea wafungwa wanaotumikia kifungo cha chini ya miezi sita na mahabusu wanaandikishwa kwa mujibu wa sheria.
“Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, sasa ni mzunguko wa tatu katika Awamu ya Pili ya uboreshaji wa Daftari. Mzunguko huu unahusisha magereza ambapo tunaboresha Daftari kwa wafungwa na mahabusu. Sheria baada ya kurekebishwa inahitaji wafungwa wenye kifungo kisichozidi miezi sita na mahabusu waruhusiwe kupiga kura”
“Mpaka kufikia kupiga kura ni mchakato, tunachofanya sasa ni kuboresha taarifa za wapiga kura na kuwaandikisha wengine wapya.Zoezi hili linahusisha vituo 140 kwa Tanzania nzima, vituo 10 kwa Tanzania Zanzibar na vituo 130 vya Tanzania Bara”
Ameongeza kuwa jana alitembelea magereza ya Bukoba, Muleba na Biharamulo katika Mkoa wa Kagera, gereza la Chato kwa Mkoa wa Geita na Gereza la Kahama na Shinyanga kwa Mkoa wa Shinyanga na ataendelea kukagua vituo vya magereza vilivyopo katika Mkoa wa Simiyu”
Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema kuwa mwamko kwa wenye sifa za kuandikishwa kwenye vituo vya magereza ni mkubwa na zoezi limerahisishwa kutokana na utaratibu mzuri uliowekwa na Jeshi la Magereza wa kuandikisha wafungwa na mahabusu na uboreshaji wa taarifa zao.
“Mwamko upo nimekuta kila kituo utaratibu mzuri umeandaliwa na Magaereza, kwa kuwa wahusika wapo sehemu maalum kwa pamoja zoezi linakwenda vizuri zaidi kuliko uboreshaji wa Daftari kwenye awamu nyingine zilizopita.”, amesema Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele.
Akizungumzia uboreshaji wa Daftari kwenye vyuo vya mafunzo Tanzania Zanzibar, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema amefanya mawasiliano na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchuguzi Mhe. Jaji Mstaafu Mbarouk Salim Mbarouk, ambaye anaongoza timu ya Zanzibar, naye pia amesema kwenye vyuo vya mafunzo zoezi linaendelea vizuri kama ilivyo kwa Tanzania Bara.
Amefafanua kuwa kwenye mikoa mingine ambako wajumbe wengine wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wanafuatilia uboreshaji wa Daftari magerezani, zoezi hilo linaendelea vyema na kwamba inawezekana ndani ya siku mbili hadi tatu zoezi hilo litakamilika lakini vituo vitakuwa wazi hadi tarehe 4 Julai, 2025.
Kwa upande wake Mwendesha Kifaa cha Bayometriki katika Kituo cha Gereza la Geita Bw. Magoti Mfungo amesema zoezi linakwenda vizuri ambapo wafungwa na mahabusu wanaoshiriki kujindikisha au kuboresha taarifa zao wamefurahi kwa kuwa litawapa fursa ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
“Katika zoezi hili ambalo tumeanza jana mpaka sasa tunaendelea vizuri, hakuna changamoto kubwa isipokuwa changamoto ndogondogo za kawaida. Mwitikio ni mzuri kwa sababu wateja wetu wote wanajiandikisha na wanashukuru kwa kuwa wamepata fursa nzuri ya kujiandikisha na watatumia haki ya kimsingi ya kupiga kura” amesema Bw. Mfungo.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeanza uboreshaji wa Daftari Awamu ya Pili mzunguko wa tatu kuanzai tarehe 28 Juni, 2025 na inatarajia kukamilisha zoezi hilo tarehe 4 Julai, 2025. Kaulimbiu ya Uboreshaji wa Daftari ni “Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura Ni Msingi wa Uchaguzi Bora”.