Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele asisitiza umuhimu wa kuwepo mawakala wa vyama vya siasa wakati wa uboreshaji wa Daftari

Imewekwa: 07 Mar, 2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele asisitiza umuhimu wa kuwepo mawakala wa vyama vya siasa wakati wa uboreshaji wa Daftari

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesisitiza umuhimu wa kuwepo mawakala wa vyama vya siasa wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiag Kura

Amesema uwepo wa mawakala wa vyama vya siasa wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni kielelezo cha uwazi na ni muhimu kwa kuwa mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.

Mhe. Jaji Mwambegele ameyamesema hayo wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa mkoa wa Dar es Salaam.

Jaji Mwambegele amesema licha ya umuhimu huo mawakala hao wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni.

“Wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura.  Jambo hili ni muhimu kwani litasaidia kuletauwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima,” amesema.

Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele amesema Tume imetoa kibali kwa asasi za kiraia 157 kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura na kibali kwa taasisi na asasi za kiraia 42 kuwa waangalizi watakaoshiriki katika zoezi la uboreshaji wa Daftari ambapo kati ya hizo, taasisi tisa ni za kimataifa na 33 ni za ndani ya nchi.