Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wananchi na wadau wote wa uchaguzi kupuuza taarifa ya upotoshaji ya uongo inayosambaa katika mitandao ya kijamii

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wananchi na wadau wote wa uchaguzi kupuuza taarifa ya upotoshaji ya uongo inayosambaa katika mitandao ya kijamii inayodai kwamba, mfumo wa Data za uchaguzi unaotumiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi umeunganishwa na mfumo wa NIDA na Chama kimoja cha Siasa na kwamba zoezi la upigaji kura (uchaguzi) limeshamalizwa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Ndg. Ramadhani Kailima kupitia Taarifa kwa Umma iliyotolewa na Tume leo tarehe 23 Agosti, 2025, na kueleza kwamba taarifa hiyo siyo sahihi na anayesambaza uongo na upotoshaji huo ana lengo la kuzua taharuki na upuuzwe kama wapotoshaji wengine.
“Ipo taarifa ya upotoshaji ya uongo inayosambaa katika mitandao ya kijamii inayoeleza kwamba, mfumo wa Data za uchaguzi unaotumiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi umeunganishwa na mfumo wa NIDA na Chama kimoja cha Siasa na kwamba zoezi la upigaji kura (uchaguzi) limeshamalizwa.” Amesema Ndg. Kailima na kufafanua kuwa:
“Napenda kutoa taarifa kwamba, Taarifa hiyo siyo sahihi, ni upotoshwaji na uongo kwa sababu zifuatazo.
Taarifa hizo za uongo na upotoshaji zinaenezwa na mtu ambaye hana uelewa na ufahamu kuhusu mfumo wa uchaguzi.
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura halijaunganishwa na mfumo wowote wa Serikali au wa Taasisi binafsi kwa madhumuni ya upigaji kura.
Mfumo wa upigaji wa kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo hautumii mfumo wa aina yoyote wa kielektroniki.
Mfumo wa upigaji wa kura, kuhesabu kura na kutangaza hutumia utaratibu wa kawaida (manual).
Baada ya kukamilika kwa zoezi la uboreshaji wa Daftari, vyama vya siasa vilikabidhiwa Daftari husika linaloonesha idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika kila kituo.
Mawakala wa upigaji kura kutoka kwenye vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi hutumia Daftari husika kuweza kumtambua mpiga kura anayefika kituoni kwa ajili ya kupiga kura.
Mfumo wa upigaji kura kwa Tanzania, mtu aliyeandikishwa hufika mwenyewe katika kituo cha kupigia kura na kuonesha kadi yake ya mpiga kura iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambapo jina lake husomwa kwa sauti na msimamizi wa kituo ili kuwawezesha mawakala wa upigaji kura kujiridhisha iwapo mtu huyo yupo katika Daftari walilopewa, baada ya uhakiki huo ndipo mhusika hupewa karatasi za kura ili aendelee na utaratibu wa kupiga kura, na
Ifahamike kuwa Kitambulisho cha Taifa hakitumiki kupigia kura, bali Kadi ya mpiga kura pekee iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na kuhakikiwa ndiyo inayotumika wakati wa upigaji kura katika vituo vya kupigia kura.
Tume inawasihi wananchi na wadau wote wa uchaguzi kupuuza uongo na upotoshaji huo, na anayesambaza ana lengo la kuzua taharuki na upuuzwe kama wapotoshaji wengine.
Aidha, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, 2025, Taarifa zote sahihi kuhusu Tume zitapatikana kwenye vyanzo ikiwa ni pamoja na tovuti ya Tume (www.inec.go.tz) na kurasa za Tume kwenye mitandao ya kijamii.
KURA YAKO HAKI YAKO JITOKEZE KUPIGA KURA”