Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi yawataka viongozi wa mikoa 16 kushiriki kuwaondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka viongozi wa mitaa na vijiji pamoja na wananchi kwa ujumla katika mikoa 16 inayoendelea na zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kushirikiana na watendaji wa zoezi hilo vituoni kutoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwepo katuika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Akiwa wilayani Mafia, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, ameshuhudia wenyeviti wa mitaa katika vituo mbalimbali alivyopita wakitoa taarifa za kuwaondoa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wapiga kura waliofariki
Akizungumza baada ya kutembelea vituo vya kuandikisha wapiga kura wilayani humo, Jaji Mwambegele amewapongeza viongozi wa serikali za mitaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia mkoani Pwani wanavyoshiriki katikia uhakiki wa Daftari la awali la Wapiga Kura na kubaini watu ambao wamefariki na kuwatolea taarifa ili waondolewe kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Viongozi wa hapa Mafia wamejitokeza vizuri kuja na orodha ya watu wasiostahili tena kuwepo kwenye Daftari, sasa nawasihi viongozi katika mikoa hii 16 hapa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar pale ambapo wanaona kuna mwenyeji wao amepoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura basi wasisite kuja kujitokeza na kufuta taarifa zao,”amesema Jaji Mwambegele.
Aidha, Jaji Mwambegele amesema zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa yote 16 limeanza vizuri na vituo vimefunguliwa kwa wakati na kuwataka wananchi ambao hawakupata fursa ya kujiandikisha hapo awali basi wafanye hivyo sasa ili wapate fursa ya kushiriki katika Uchaguzi Mwezi oktoba mwaka huu.
Afisa Mwadikishaji wa Jimbo la Mafia, Mohamed Hussein Othman akizungumzia zoezi hilo amesema limeanza vyema katika vituo vyote 15 ndani ya jimbo hilo na wananchi waliokosa fursa ya kujiandikisha na kuboresha taarifa zao hapo awali wanajitokeza hivi sasa.
“Zoezi letu la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura limeanza vizuri, vituo vyote 15 vimefunguliwa saa 2:00 asubuhi wananchi wanajitokeza kuboresha taarifa zao na wale ambao hawakupata fursa katika uboreshaji wa awamu ya kwanza nao wanajitokeza kuhakikisha kwamba wanakuwepo katika Dafrari la Kudumu la Wapiga Kura,”alisema Othman.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Vunjanazi kilichopo Kata ya Kilindoni Wilayani Mafia, Mwl. Omar Mngwali amesema yeye amekua kiongozi katika kitongoji hicho kwa muda mrefu na kushiriki vyema katika shughuli za kijamii imemuwezesha kutambua watu wake waliofariki wapatao 11 na kutoa taarifa ili waondolewe kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mzunguko wa pili wa uboreshaji umeanza leo Mei 16 na utaenda hadi Mei 22, 2025 unahusisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba ambapo zoezi hilo litafanyika kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025.
Zoezi hilo linakwenda sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la awali la Wapiga Kura ambapo wananchi wanapata fursa ya kukagua, kufanya marekebisho ya taarifa za wapiga kura na uwekaji wa pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye Daftari ambao hawana sifa na limebandikwa katika vituo vyote vilivyotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza.