Tume yaruhusu wapiga kura kutumia simu ya kiswaswadu kuboresha au kuhamisha taarifa zao kwenye Daftari

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeruhusu wapiga kura waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, wanaotaka kuboresha au kuhamisha taarifa zao kutoka jimbo au kata moja kwenda jimbo au kata nyingine kutumia simu ndogo za kitochi au kiswaswadu kuanzisha mchakato wa uboreshaji wa Daftari.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Tume na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani, uamuzi huo wa Tume umetokana na maoni ya wadau wa uchaguzi.
“Tume imefanyia kazi maoni na ushauri huo (wa wadau) na kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 watu wote wenye simu za kawaida (maarufu kama kitochi au kiswaswadu) na watahitaji kuboresha au kuhamisha taarifa zao, watapata huduma hiyo kwa kupiga USSD Code *152*00# na kubonyeza namba 9 kisha kuendelea na hatua zingine kama itakavyokuwa inaelekezwa kwenye simu husika,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa mpiga kura anayetumia njia hii atapokea namba maalum (token) kupitia simu yake kisha atalazimika kwenda na namba hizo kwenye kituo anachotarajia kutumia kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ili kukamilisha mchakato na kupewa kadi mpya.
Katika hatua nyingine, Tume imetoa taarifa kwa umma kuhusu kuanza rasmi kwa kituo cha huduma kwa mpiga kura (Call Centre) kinachoanza kutoa huduma kuanzia leo Alhamis tarehe 18 Julai, 2024.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Bw. Kailima, huduma hiyo ni ya bure na itatolewa kwa saa 14 kila siku kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 2:00 usiku.
“Kupitia kituo hiki wananchi watapata fursa ya kupiga simu bila malipo kupitia namba 0800112100 na kupata majibu au ufafanuzi wa maswali au jambo lolote linalohusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hivyo, wananchi wote mnakaribishwa kutumia huduma hii kwa kipindi chote cha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Kwanza unazinduliwa Siku ya Jumamosi tarehe 20 Julai, 2024 Mkoani Kigoma katika Uwanja wa Kawawa na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb).