Tume yatangaza Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Kwahani utakaofanyika Juni 8, 2024

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Kwahani lililipo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar utakaofanyika siku ya Jumamosi tarehe 8 Juni mwaka 2024.
Uchaguzi huo umetangazwa tarehe 2 Mei, 2024 Jijini Dodoma kupitia taarifa kwa umma iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima, R. K baada ya Tume kupokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akimtaarifu Mwenyekiti wa Tume kuhusu uwepo wa nafasi wazi ya ubunge katika jimbo hilo.
Bw. Kailima alisema katika taarifa hiyo kuwa, kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi huo mdogo fomu za uteuzi zitatolewa kuanzia tarehe 17 hadi 23 Mei, 2024, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 23 Mei, 2024, wakati kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 24 Mei, 2024 hadi tarehe 7 Juni, 2024 na siku ya uchaguzi itakuwa tarehe 8 Juni, 2024.
Aliongeza kuwa, Tume inavikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi cha uchaguzi huo mdogo.
Alifafanua kuwa Spika alitoa taarifa hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 49(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka, 2024.
Alisema Tume imeitangaza uchaguzi huo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 49(1)(b) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024..
Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Kwahani, Zanzibar umetangazwa kufuatia kifo cha mbunge wa jimbo hilo Mhe. Ahmed Yahya Abdulwakil, kilichotangazwa tarehe 8 Aprili, 2024 na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.