Tume yawataka vijana kutumia majukwaa, taasisi na mashirika yao kuhamasishana kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa wito kwa vijana kutumia majukwaa, taasisi na mashirika yao kuhamasishana kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa Tume na wawakilishi wa vijana uliofanyika leo tarehe 11 Juni, 2024 jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mkutano huo umefanyika sambamba na mkutano wa Tume na wawakilishi wa wanawake na wawakilishi wa watu wenye ulemavu ikiwa ni mwendelezo wa mfululizo wa vikao kama hivyo vilivyofanyika kuanzia tarehe 07 Juni, 2024.
"Wawakilishi wa vijana mnayofursa ya kuwahamasisha vijana wenzenu kwenye majukwaa yenu. Hivyo, tunawasihi na kuwaomba kwa dhati mtumie fursa hizo wakati wote mnapotangaziana mambo mbalimabli, moja ya matangazo yawe kuwahamasisha vijana kujitokeza kujiandikisha kuwa wapiga kura," amesema.
Jaji Mwambegele amewashukuru wawakilishi wa vijana kwa ushirikiano mkubwa ambao wameuonesha kwa Tume wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.
"Kwenye mazoezi ya uboreshaji wa Daftari yaliyopita, vijana mmekuwa msaada mkubwa katika kuhamasisha na kuelimisha wananchi haswa kundi lenu la vijana kupitia majukwaa mbalimbali," amesema.
Jaji Mwambegele pia amewashukuru vijana kwa kujitokeza kwa wingi kiasi ambacho kimeiwezesha Tume kufikia malengo yake ya kuandikisha wapiga kura na kuwaomba waendelee na utamaduni huo.
Akiwasilisha mada yake kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima R. K amesema uboreshaji wa daftrai pamoja na mambo mengine utahusu kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Ameongeza kuwa zoezi hilo pia Iitatoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye daftari na ambao wamehama, waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo walioandikishwa awali.
Zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linatarajiwa kuzinduliwa tarehe 01 Julai, 2024 katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma.