Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Watendaji wa Vituo vya Kupigia Kura Chamwino waaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia sheria

Imewekwa: 01 Nov, 2026
Watendaji wa Vituo vya Kupigia Kura Chamwino waaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia sheria

Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima, leo Novemba 1, 2026, ametembelea mafunzo ya Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Vituo vya Kupigia Kura katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Chamwino, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Chamwino, mkoani Dodoma.

Ziara hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino, unaotarajiwa kufanyika Jumatano, Novemba 4, 2026.

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Kailima amewasisitiza kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru na haki.

Kailima amewataka wasimamizi hao kudumisha ushirikiano na mawakala wa vyama vya siasa katika vituo vya kupigia kura kwa kuwafahamisha wajibu na mipaka ya majukumu yao, huku akisisitiza umuhimu wa wasimamizi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu rasmi badala ya kupokea maelekezo kutoka kwa mawakala.

Uchaguzi huo utafanyika sambamba na Uchaguzi Mdogo wa Madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara.

Kata hizo ni Nonde iliyopo Halmashauri ya Jiji la Mbeya; Lugenge, Halmashauri ya Mji Njombe; Bargish, Halmashauri ya Mji Mbulu; Makole, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza; Mwera, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani; na Oldonyosambu, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Kata nyingine ni Igalula iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui; Shelui, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba; Mvumi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa; Nyarero, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime; na Ilolangulu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.