Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Watendaji wa Uchaguzi watakiwa kuepuka kufanya kazi kwa mazoea

Imewekwa: 28 Apr, 2026
Watendaji wa Uchaguzi watakiwa kuepuka kufanya kazi kwa mazoea

Watendaji wa uchaguzi wametakiwa kuepuka kufanya kazi kwa mazoea licha ya baadhi yao kuwa na uzoefu kwenye masuala ya uchaguzi.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele leo tarehe 28 Aprili, 2026 mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya uchaguzi mdogo wa ubunge kwenye Jimbo la Ismani Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Mkoani Iringa na Kata 12 za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika tarehe 01 Juni, 2026.

“Nachukua nafasi hii kuwaasa kuwa, pamoja na uzoefu ambao baadhi yenu mnao katika uendeshaji wa uchaguzi, mhakikishe mnazingatia maelekezo mtakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea. Kwani kila uchaguzi unatofautiana na uchaguzi mwingine,” amesema Jaji Mwambegele.

Ameongeza kuwa watendaji hao wa uchaguzi wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo watakayopewa na Tume ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanavishirikisha vyama vya siasa katika hatua zote kuelekea uchaguzi huo.  

 “Wakati wote wa mchakato wa uchaguzi huu, ni vema mkavishirikisha kwa karibu vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yenu kuhusu masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia utekelezaji wa majukumu yenu,” amesema Jaji Mwambegele.

Amewataka watendaji hao kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika na kuhakikisha kunakuwa na mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.

Jaji Mwambegele amewasisitiza watendaji hao kuhakikisha wanaajiri watendaji wa vituo wenye sifa, weledi, wanaojitambua na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.

“Mhakiki vifaa vya uchaguzi mnavyopokea kutoka Tume na kuhakikisha kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote vya uchaguzi vinavyohitajika mapema na muweke utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 asubuhi,” amesema.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamewahusisha Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Ngazi ya Jimbo, Wasimamizi wa Uchaguzi Ngazi ya Kata, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ununuzi na Wahasibu.

Kata 12 za Tanzania Bara zitakazofanya uchaguzi wa Udiwani ni Mzimuni iliyopo Manispaa ya Kinondoni; Zongomera, Manispaa ya Kahama; Itilo, Halmashauri ya Mji wa Nzega; Ketare, Halmashauri ya Mji wa Tarime na Nyumbigwa, Halmashauri ya Mji wa Kasulu.

Nyingine ni kata ya Kala iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi; Ziba, Halmashauri ya Wilaya Igunga; Kamsisi, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele; Nyamugali, Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe; Namasakata Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru; Bwongera, Halmashauri ya Wilaya ya Chato na Kibiti Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.