Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Watumishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba, sheria, kanuni na taratibu

Imewekwa: 12 Apr, 2026
Watumishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba, sheria, kanuni  na taratibu

Watumishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba, sheria, kanuni na taratibu na kuepuka lugha zozote za uchochezi zinazoweza kuleta uvunjifu wa amani na kuhatarisha maisha ya Watanzania. Hayo yamesemwa leo Aprili 11, 2026 na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu), Dkt. James Henry Kilabuko kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Jimmy Yonaz wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, katika kikao kilichoketi Mkoani Morogoro. “Napenda kuwaasa, kuzingatia katiba, sheria, kanuni na taratibu mnapotekeleza majukumu ya Tume na kuepuka lugha zozote za uchochezi zinazoweza kuleta uvunjifu wa amani na kuhatarisha maisha ya Watanzania,”amesema Dkt. Kilabuko. Dkt. Kilabuko ameongeza kuwa, taasisi ina malengo yake, upo uwezakano wa kuepusha migogoro ya ndani na nje ya taasisi inayoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa ufanisi. Mapema akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi INEC ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Ndg. Kailima, R. K amesema kwa sasa Tume inaendelea na zoezi la kuandaa Taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2025. “Tume imekamilisha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 ambao ulifanyika tarehe 29 Oktoba, 2025. Kwa sasa Tume inaendelea na zoezi la uandishi wa Taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2025 ,”amesema Kailima. Aidha, amesema Tume ipo katika maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Isimani mkoani Iringa kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. William Lukuvi pamoja na uchaguzi wa udiwani katika Kata mbalimbali nchini ambazo madiwani wake walifariki. Kikao hicho cha siku moja pia kilitumika kufanya uchaguzi wa Katibu wa Baraza hilo ambapo wajumbe walimchagua Ndg. Mwitaru Keboya kuwa Katibu mpya wa Baraza akichukua nafasi ya Ndg. Livini Avith ambaye amemaliza muda wake.